Pages

Pages

Monday 5 January 2015

Historia ya Fasihi ya Kiswahili ina uhusiano gani na historia ya lugha yaKiswahili?



Kwa mujibu wa Eagleton (1983: 1 – 8) Fasihi ni tokeo la masimulizi ya lugha kwa  njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalum.
 Fasihi ni sanaa ya lugha  yenye ubunifu inayojaribu kusawiri vipengele vya maisha, na mahusiano na hisia za watu katika muktadha fulani (Mulokozi, 1996).
 kwa mujibu wa Mazingwe 1991:18 & Siyambo na Mazrui (1992) wanasema kwamba fasihi ya Kiswahili ni  fasihi yote inayoelezwa kwa lugha ya Kiswahili hivyo, wataalamu mbali mbali wameonesha kuwa kuna aina mbili za fasihi ya Kiswahili nazo ni : Fasihi simulizi na fasihi Andishi.
 Vile vile lugha ya Kiswahili asili yake ni upwa wa Afrika mashariki inayozungumzwa zaidi na waswahili, yenye utamaduni wake wa Kiswahili na pia iliyosanifiwa kutokana na mchanganyiko na lahaja.
 Baada ya kuangalia maana ya fasihi na lugha ya Kiswahili tunaangalia mswahili ni nani? Hii ni kwa sababu ikiwa lugha  ya Kiswahili ipo  bila shaka  waswahili  pia wapo, haiwezekani kabisa kuwepo kwa  lugha ya Kiswahili bila ya kuwepo waswahili .
      Mswahili ni mtu yeyote ambaye anaishi mwambao wa Afrika mashariki na visiwa vyake, anayezungumza Kiswahili ikiwa ni lugha yake ya kwanza, aidha mswahili ni mtu aliyetokana  na jamii ya watu wa mwambao wa afrika Mashariki na kuendeleza utamaduni wa mswahili, hii ikiwa ni pamoja na kucngumza lugha fasaha.
Kutokana  na maelezo hayo ni dhahiri kwamba, madai ya baadhi ya watu kuwa hakuna waswahili hayakubaliki. Pia historia ya lugha ya Kiswahili inaendelea kueleza kuwa waswahili wapo na walikuwepo tangu karne nyingi, walijiita kwa majina mbali mbali mfano waamu, Wapate, Wamvita, Wapemba, Waunguja n.k. Hata hivyo waliunganishwa kwa lguha  moja na utamaduni mmoja. Wataalamu wanaendeleza kueleza kuwa waswahili walikuwepo tangu karne nyingi na wapo hadi sasa wana lugha yao ya Kiswahili na bila shaka wanayo fasihi yao ya Kiswahili.
Fasihi ya Kiswahili ilikuwepo tangu kuwepo kwa mswahili. Aidha baadhi ya fasihi ya mwanzo  kabisa  ni pamoja na utenzi wa Fumo Lyongo na nyimbo mbali mbali za shughuli za kijamii ambazo ziliimbwa kwenye sherehe, harusi, jando na unyago au katika shughuli za kiuchumi kama vile shughuli za kilimo na uvuvi.
Wataalamu wanaendelea kueleza kuwa waswahili ni wenyeji wa mwambao wa kaskazini kuanzia Barawa (Somalia) hadi Tanga, wenyeji wa mwambao wa kusini na visiwa vyake.
Kuenea kwa lugha ya Kiswahili katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki kumeifanya lugha hiyo iwe chombo cha fasihi ya watu wote wanaoitumia, hivyo basi fasihi ya Kiswahili na lugha ya Kiswahili vilikuwepo na  vilitumika kwa karne nyingi zilizopita hadi sasa. Fasihi hiyo ndio tutakayoita Fasihi ya Kiswahili (Siyambo na Mazrui – 1992).
Kutokana na maelezo hayo ni dhahiri kuwa fasihi ya Kiswahili ilikuwepo tangu kuwepo kwa lugha ya Kiswahili na hii inaonesha kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ni kama ufuatao
           Kwanza, historia ya fasihi ya kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili chimbuko lake ni  upwa wa Afrika Mashariki. Historia inaonesha kuwa fasihi ya Kiswahili chimbuko lake ni upwa wa Afrika Mashairki hii ni kutokana kuwa hapo awali jamii  kama Wangoni, Waamu, Wapate, jamii hizi zilipatikana katika Upwa wa Afrika mashariki ambapo hawakufahamu jinsi ya kuandika fasihi katika maandishi, kwa sababu zilikuwepo fasihi zao za jadi katika mapokezi (yaani fasihi simulizi), hivyo walipowasili Waarabu ndipo walipoanza kuandika fasihi zao katika maandishi. Na kutokana na ushahidi huo inaonesha kuwa fasihi ya Kiswahili ilikuwepo tangu zamani kabla ya kuja kwa wageni mfano wa fasihi hizo ni utenzi wa FumoLyongo, mashairi ya Inkishafi nakadhalika. mfano wa utenzi wa Fumolyongo ni:-
                        Liyongo kitamkali,
                        Akabalighi rijali,
                        Akawa mtu wa kweli,
                        Na haiba huongea.
Kwa upande wa historia ya lugha ya Kiswahili  tunaona pia chimbuko lake ni Upwa wa Afrika Mashariki, na haikuletwa, na  wageni  kama nadharia nyengine zinavyodai isipokuwa inasemekana waliunganisha lugha  ambazo zilikuwepo na  kuziita jina moja tu nalo ni Kiswahili. Hii ni kutokana  na ushahidi mbali mbali unaoonesha kuwa lugha ya Kiswahili ilikuwepo tangu zamani na ilikuwa ikizungumzwa na jamii mbali mbali za  Afrika Mashariki mfano Wapate, Wangoni na Waamu, kama ni jamii za awali zilizozungumza Kiswahili. Hivyo kutokana na jamii hizo ushahidi kama wa tenzi mbali mbali zilizopatikana ambazo zinaonesha kuwa kweli Kiswahili kilikuwepo. Hivyo kutokana  na ushahidi huo ni kweli kuwa upo uhusiano kati ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili.Kwa hiyo tunaona kuwa historia ya fasihi ya Kiswahili ndio iliotumika kama ushahidi wa kuthibitisha kuwa kweli lugha ya Kiswahili chimbuko lake ni upwa wa Afrika mashariki, kama wataalamu mbali mbali walivyothibitisha kutokana na ushahidi madhubuti kama wa fumoliyongo.
        Vile vile uhusiano mwengine ni kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na waarabu  pamoja na Uislamu. Hii ni kutokana na historia ya fasihi ya Kiswahili katika sehemu ambazo zilichimbuka fasihi ya Kiswahili kama jamii za wapate, wangoni, Waamu, hawa hawakuweza kuandika fasihi  katika maandishi na hivyo  katika mwaka 1670 waarabu walipofika katika Upwa wa Afrika Mashariki walianza kuandika katika maandishi na inaaminika kuwa miongoni mwa maandishi ya mwanzo ni utenzi wa Hamziyya ambao uliandikwa mwaka 1670, ambao ulikuwa ni wa kidini. Hamziyya unahusu maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) mfano:-
                        “Akusudia, Mustwafa kwenda Madina
                        Makka jina lake, zikaleta kushukuru mema”
Pia utenzi wa Tambuka ambao umezungumzia juu ya vita vikali vya Uislamu wa mwanzo wa mfalme Herekali wa Dola ya Warumi (Mulokozi, 1996). Mfano wa beti ya utenzi wa Tambuka.
                        “Bismilahi kutubu
                        Jina la Mola wahabbu
                        Arra  Amani eribu
                        Na arraimu ukyowa”
 Pamoja na utenzi wa al- Inkishafi na utenzi wa Mwanakupona (Mulokozi 1999). Mfano wa beti ya utenzi wa Mwanakupona unaozungumzia dini ya kiislamu.
                        “La kwanda kamata dini
                        Faradhi usiikhini
                        Na sunna ikimkini
                         Ni wajibu kuitia……(ubeti 12
Vile vile, tenzi ambazo zinazungumzia uislamu ziliendelea hadi wakati wa Muyaka bin Haji (1770 – 1840) na pia yeye ndie aliyebadilisha mtindo  huu wa kidini na akaanzisha wake ulikuwa unazungumzia mambo mengine tofauti (na kama inavyosemekana yeye ndiye alioutoa ushairi msikitini na kuupeleka sokoni).

            Katika historia ya lugha ya Kiswahili pia imeathiriwa na waarabu na pamoja na uislamu. Kwani historia ya lugha inaonesha kuwa waarabu ndio walioanzisha maandishi ya Kiswahili kwa hati za kiarabu pamoja  na utamaduni wa mswahili  na ustaarabu wao unaohusishwa na uislamu. Kutokana na mchanganyiko mkubwa uliokuwepo baina ya  waswahili na waarabu katika utamaduni wao ni dhahiri kuwa fasihi zao zilikuwa zinazungumzia uisilamu kwa sababu  hizo ni dhahiri kwamba historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili  zina uhusiano mkubwa kutokana na utamaduni wa Kiswahili uliodhihirishwa na waarabu na uislamu ndio uliopelekea fasihi hizo za awali kuzungumzia zaidi mambo ya uislamu. Hivyo  kutokana na historia ya fasihi ya Kiswahili  kuathiriwa na uislamu, ndio iliyopelekea kuwa fasihi za awali za Kiswahili kuzungumzia zaidi masuala ya dini ya kiislamu na kupelekea katika utamaduni wa lugha ya Kiswahili na waswahili kuwa ni wa kiislamu.

            Uhusiano mwengine kati ya historia ya lugha ya Kiswahili na historia ya fasihi ya kiswahili ni kukua na  kuimarika zaidi katika maeneo mengi ambayo kihistoria yalikaliwa sana na wageni  ukilinganisha na maeneo ambayo hayakukaliwa sana na wageni. mfano wa maeneo ambayo yalikaliwa sana  na wageni ni Pate, Lamu, Mombasa, Zanzibari na Tanga (Samuel na wenzake 2013) .Katika maeneo hayo kulitokea watu mbali mbali wenye vipawa vikubwa katika kazi nyingi za fasihi na kupata umaarufu mkubwa  sana kote Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, mfano:-

            Pate, walitoka washairi maarufu kama vile Sayyid Abdalla bin Nassir Mwanakupona binti Msham, Nabhani, Fumoliyongo, Ali Athumani Koti, Mohammed bin Sheikh Malaka.
Mombasa – Ahmeid Nassor bin Bhalo .
Lamu – Muhamed Abubakar Kijumwa, Ahmeid Sheikh Nabhan, Zahid bin Mngumi, Tanga – Hemed bin Abdalla Albuhri, Ghulam Mabondo bin Mwinyimatano, Swaleh Kibwana na Shaaban Robert.
Zanzibar – Siti binti Saadi, Yahya Burhan, Said A. Mohammed na Shafi Adam Safi. Historia hii na mahala wanapotoka wanafasihi hawa imeelezwa na Mulokozi na Sengo 1995.

            Pia, historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili zimeibuka kupitia masimulizi. Historia ya fasihi ya Kiswahili ilizuka kwa masimulizi ambayo yalikuwa yakitumia lugha ya mazungumzo ndipo zikaibuka hadithi fupi fupi.
Kwa  mujibu wa Holman (1992) anasema kwamba hadithi fupi ni masimulizi mafupi ya kubuni katika mtindo wa nathari. Baadhi ya fani ambazo ziliathiri kuchipuka kwa hadithi fupi ni ngano, hekaya, rara, utendi na riwaya chuku.
Katika historia ya lugha ya Kiswahili kuna ithibati ya kutumika Kiswahili kabla ya kuja kwa wageni, kuna ushahidi wa kimasimulizi ambapo wenyeji waliweza kusimulia. Mfano wa masimulizi hayo ni kisa cha Anzaruni kilichoandikwa na binti Lemba (1663),  siri al – as – rar iliyoandikwa na Kadhi Kassim bin Jaffar, pia wakati wa ukoloni kulikuwa na hadithi za Wayunani(1889), Mchawi(1900), H.R Haggad na safari za wasafiri (1925). iliyoandikwa Bunjan.
            Hivyo basi uhusiano baina ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ziliibuka kupitia masimulizi. Mfano:- tendi, rara, hekaya riwaya chuku ambazo walikuwa wakizisimulia,
            Pia,  uhusiano mwengine uliojitokeza  ni kwa kukua kwa matumizi ya lugha. Lugha imeanza mara tu, mwanaadamu alipoanza kuyakabili mazingira yake katika nyanja za kiuchumi na  kijamii. Hicyo watu walikuwa wakiitumia lugha katika shughuli mbali mbali. Kwa minajili hiyo tunaweza kusema kwamba historia ya lugha ya Kiswahili ndio iliyopelekea kuibuka kwa fasihi ya Kiswahili. Mfano kupitia katika jamii walikuwa wakitumia nyimbo kama vile wimbo wa “Nabhan” mfano.
                        “Ndiwa wangu,                       Sindiwa wa mabaoni.
                        Ndiwa wangu,                        Ni mweupe wa Launi.
                        Ndiwa wangu             Ushabihi wa peponi.”
Kwa upande wa kiuchumi kulikuwa na  wimbo wa “WAWE”

Wawe – Ni utungo ambao huimbwa kwa kujitayarisha na shughuli za kilimo mfano wa beti wa ushairi ni:-
                        “N’kasiye, N’kalima ,                         N’kavuna.
                        Masika yenye makame,           Chini yaliyojificha.
            N’kafyeka, N’kachoma,          moto ukajirimbika”.
            Hivyo,  tunaona wazi kwamba historia ya fasihi ya Kiswahili inaonekena zilizuka kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii ndipo tunapopata  uhusiano mkubwa baina ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili.

            Hata hivyo, uhusiano uliopo baina ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ni kwamba zote ni fasihi ambazo huonesha sehemu ya utamaduni wa jamii kama vile historia  ya lugha ilivyo sehemu ya utamaduni yenye kueleza au kuitazamia jamii kiutamaduni, kiuchumi, kiufundi na kisiasa vile vile uhusiano huu  huwa ni darubini ya kuitazama mfumo wa maisha ya jamii yoyote ikiwa ni ya kikabila au ya  kibepari au ya kijamii.

Kwa kuhitimisha suali letu, tunaweza kusema kuwa historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya kiswahili zina uhusiano mkubwa na kwamba dhana mbili hizi haziwezi kutenganishwa kutokana na ukweli kwamba zinategemeana kwa kila hali, zinajengana na kuathiriana sana . Kuwepo kwa  dhana moja kulipelekea kujitokeza kwa dhana nyengine. Hivyo ndio kusema kwamba ,ni rahisi kuisoma na kuielewa historia ya fasihi ya Kiswahili iwapo tutaisoma na kuielewa historia ya lugha ya Kiswahili kama vile ambavyo ni rahisi kuisoma na kuielewa historia ya lugha ya Kiswahili iwapo tutaisoma na kuielewa historia ya fasihi ya Kiswahili.











MAREJEO
Samwel ,M & Seleman A,J &Kabiero A,J(2013) Ushairi wa Kiswahili :Nadharia  ,mwongozo kwa walimu wa Kiswahili na diwani MEA, DSM .MVP
                                                                                                                        
TUKI(1983) Makala za seminar za kimataifa ya waandishi wa Kiswahili 111-Fasihi, DSM:DUP

Mulokozi,M,M(1999) Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili Dar-es-Salaam :chuo kikuu cha Dar-es- Salaam

Mulokozi ,M,M (19 96)utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili Dar-es-Salaam:Tuki

Maganga,C(1997) Historia ya Kiswahili ,Dar-es-Salaam:Chuo kikuu huria cha Tanzania





1 comment:

  1. Mmefanya kazi nzuri ambazo zinatuelekeza kujua Kiswahili nchini Rwanda

    ReplyDelete