HISTORIA
NA MAENDELEO YA LUGHA YA KISWAHILI
MIONGONI MWA PWANI ZA AFRIKA MASHARIKI |
Ili kuweza kufahamu
historia na maendeleo ya Kiswahili inatupasa kufahamu maana ya Msawahili na
Kiswahili. Mswahili ni nani? Ni swali ambalo ni la mjadala kwani baadhi ya
wataalamu wamejaribu kulifafanua suala hili kwa mitazamo tafauti katika fasili
zao mbali mbali kama zifuatazo;
Maganga, C. (1997),
anasema Waswahili ni watu wazungumzao lugha ya kiafrika inayohusiana sana na
lugha za kibantu zinazozungumzwa hivi sasa kando mwa pwani ya Kaskazini ya
Kenya, Somalia na kwamba ilingiza maneno mengi ya Kiarabu katika karne chache
zilizopita.
Massamba, D. (2002),
akimnukuu Stigand, (1913), Waswahili ni watu waliotokana na uzao wa umoja wa
Waarabu au Waajemi wa asili waliotamakani katika upwa wa Afrika ya Mashariki.
Massamba, D. (2002),
Waswahili ni watu wanaoishi katika eneo la mji ambako huishi watu wa kawaida
(wa hali ya chini) hii ilitokana na hali halisi ya matabaka yaliyokuwa
yakijitokeza katika miji ya pwani baada ya kufika kwa wakoloni ( wa Kiarabu na
Kizungu) na wafanya biashara wa Kihindi.
Kwa ujumla tunaweza
kusema kuwa Waswahili ni watu wa upwa wa Afrika ya Mashariki ambao lugha yao ya
mawasiliano ni Kiswahili.
Kwa maana hiyo
Kiswahili ni lugha inayotumiwa na watu wa upwa wa Afrika Mashariki katika
shughuli zao zote za mawasiliano.
Baada ya kufahamu
maana ya Kiswahili na Mswahili tunapaswa kufahamu vyanzo mbali mbali ambavyo
tunaweza kutumia kupata historia ya Kiswahili kama ifuatavyo. Kuna vyanzo kama
vya kihistoria, Kiakolojia, Kijiografia, Kiisimu au Kilughawiya na vyenginevyo.
Kabla ya kujadili
asili ya lugha ya Kiswahili ni muhimu kufahamu maana ya neno asili.
Kwa mujibu wa
Massamba na wenzake (1999), neno asili lina maana ya jinsi kitu au jambo
lilivyotokea au lilivyoanza. Kuna nadharia mbali mbali zinazozungumza juu ya
asili ya Lugha ya Kiswahili kama vile Kiswahili ni Kikongo, Kiswahili ni
Kiarabu, Kiswahili pijini au Krioli, Kiswahili ni Kibantu na nyenginezo.
Kuhusu nadharia ya
Kiswahili ni Kikongo baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya Kiswahili ni huko
Kongo ambayo ni Zaire ya sasa. Dai hilo linaimarishwa na wazo jengine linalodai
kwamba katika vipindi kongwe vilivyopita, kuweko sehemu ya pwani ya Afrika ya
Mashariki hazikuwa zimekaliwa na watu. Kutokana na vita uchungaji na biashara,
inadaiwa kuwa Wabantu walitokea sehemu za Kongo na walisambaa na kuja pwani ya
Afrika Mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya Wabantu hawa walipitia sehemu za
Uganda wakati wa kusambaa kwao walieneza pia lugha zao ikiwemo hii ya Kiswahili
(Msokile 1992:12).
Pia kuna madai kwamba
Kiswahili ni Kiarabu. Madai hayo yanaambatana na hoja tatu kuu. Kwanza inadaiwa
kuwa asilimia 41 ya maneno yote ya Kiswahili yanayoweza kuandikwa ni asili ya
Kiarabu. Hoja ya pili inahusu neno lenyewe la Kiswahili ambalo asili yake ni
Kiarabu. Kimsingi neno “Sahil” (Umoja) lina maana ya Pwani. Swahil (wingi)
hutumika katika maana ya wingi. Na sababu ya tatu inayotolewa ni ile inayohusu
shughuli mbali mbali zilizohusishwa sana na waarabu kama vile dini, biashara,
utawala, mila na desturi.
Kadhalika kuna dai
linasema kuwa Kiswahili ni Krioli au Pijini. Nadharia ya pijini au Krioli
hutumia kigezo cha msamiati wa Kiswahili kuonesha uhusiano uliopo kati ya
Kiswahili na Kiarabu. Inadaiwa kuwa msamiati mwingi wa Kiswahili unatoka na
Kiarabu hivyo huhitimisha kuwa hapana shaka Kiarabu kimehusika katika kuzaliwa
lugha ya Kiswahili. Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa haitumii vigezo vya lugha
kama vile matamshi, miundo ya maneno na muundo wa sentensi za Kiswahili (Masebo
na mwenzake 2010).
Mbali na nadharia hizo kuna nadharia ya Kiswahili ni Kibantu. Mtazamo huu
unaamini kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu na lugha za Kibantu zilikuwepo hata
kabla ya kuja kwa wageni kutoka Ujerumani, Uarabuni, India, China na
kwengineko. Katika mtazamo huu lugha ya Kiswahili inaingizwa katika kundi la
lugha za Kibantu. Vigezo vilivyotumika kufafanua kuwa Kiswahili ni Kibantu ni
pamoja na;- Msamiati, Mofolojia, Mfumo wa Sauti, Mfumo wa ngeli na mpangilio wa
maneno. Hata hivyo kila hoja ina maelezo ya kina katika kujadili kile
wanachokiamini. Makundi mengi ya wataalamu wanaelekea kukubaliana na dai la
kuwa Kiswahili kimetokana na Kibantu kutokana na hoja mbali mbali
zilizoainishwa.
Kwa upande wa
chimbuko la lugha ya Kiswahili limejadiliwa na wataalamu wengi. Mijadala yao
imeambatana na kauli mbali mbali zinazohusu nadharia ya chimbuko la Kiswahili.
Inasemekana kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni kando kando ya upwa wa
Afrika Mashariki ambapo kuna miji mingi ya awali ambayo baadhi ya wataalamu hao
wanaamini kuwa ndio chimbuko la Kiswahili. Mifano miji hiyo ni kama vile eneo
la Mogadishu ambapo eneo hili linapatikana Kaskazini mwa mwambao wa Afrika ya
Mashari na wakaazi wake walikuwa wakitumia Kiswahili. Eneo jengine ni eneo la
Manda, na linapatikana katika visiwa vya Pate ambavyo vipo katika nchi ya
Kenya, eneo hili limethibitika kuwa linazungumza Kiswahili baada ya wasafiri
mbali mbali kutembelea eneo hilo. Vile vile katika mji wa Kilwa nako kuna
ushahidi wa miji ya kwanza kuzungumza Kiswahili. Miji mengine ni kama vile Lamu,
Mombasa, Dar-es-salaam, Bagamoyo, Tanga, na Zanzibar. Vile vile katika mji wa
Kilwa nako kuna ushahidi wa miji ya kwanza kuzungumza Kiswahili. Miji mengine
ni kama vile Lamu, Mombasa, Dar-es-salaam, Bagamoyo, Tanga, na Zanzibar.
Tukiendele na
historia ya Kiswahili kabla ya uhuru wageni walikitumia Kiswahili katika nyanja
za elimu. Elimu ilitoa mchango mkubwa katika kipindi cha ujio wa wageni. Mfano
katika kipindi cha Wajerumani waliiteua lugha ya Kiswahili kuwa itumike kama
lugha ya kufundishia na pia kusomwa kama somo la kawaida katika shule za
msingi. Baadhi ya shule hizo ni kama vile Tabora, Mpwapwa na kadhalika. Hivyo
walimu na wanafunzi walijifunza lugha ya Kiswahili katika shughuli za elimu
sambamba na kuifanya lugha hiyo kukuwa na kuenea katika maeneo tafauti. Waarabu
nao walikitumia Kiswahili ili kufundishia watoto uislamu. Hivyo misamiati mingi
ilipatikana kupitia elimu. Mfano neno Madrasa, daftari, kalamu na kadhalika
ambayo hadi leo yanatumika katika lugha ya Kiswahili. Vile vile Kiswahili
kilitumika katika nyanja za biashara.
Wageni walipofika
katika pwani ya Afrika Mashariki waliwakuta wenyeji wakizungumza lugha ya
Kiswahili. Hivyo walilazimika kutumia lugha ya Kiswahili ili kukidhi mahitaji
ya mawasiliano katika biashara zao. Katika kuhakikisha biashara inakuwa vizuri
Waarabu walianzisha vituo vya biashara kama vile Ujiji, Tabora n.k sambamba na
kuenea kwa lugha ya Kiswahili katika sehemu tafauti na kupata mawanda mapana ya
kimatumizi na watumiaji wengi.
Pia wageni walisanifisha lugha ya Kiswahili. Baada ya ujio wa
Waengereza juhudi mbali mbali zilifanywa katika kueneza Kiswahili mwanzoni mwa
miaka ya 1930 na vita vikuu vya pili vya dunia, Waengereza walifanya juhudi za
kukisanifisha Kiswahili na kukuza istilahi zake. Mfano maneno kama “Skuli”,
“Shati” n.k yote hayo yanatoka katika lugha ya kingereza. Hivyo Kiswahili
kilitumika katika shughuli rasmi sambamba na kuenea sehemu tafauti za dunia.
Hata hivyo walikitumia
Kiswahili katika shughuli za kilimo. Miongoni mwa mambo yaliyopelekea maendeleo
ya Kiswahili katika kipindi cha ujio wa wageni ni kilimo. Mfano Wajerumani
walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama vile katani huko Tanga
na kahawa huko Kilimanjaro na Bukoba. Hivyo waliajiri idadi kubwa ya vibarua kutoka
sehemu mbali mbali za nchi na lugha iliokuwa ikitumika ni Kiswahili. Hivyo
Kiswahili kilikuwa na ongezeko la watumiaji na kufanya lugha hiyo kuenea katika
maeneo tafauti.
Kadhali katika
kipindi hicho dini zote mbili Ukiristo na Uislamu ni miongoni mwa sababu
zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kueneza Kiswahili nchini. Kabla ya
uhuru hadi sasa. Dini zote mbili huendesha mahubiri yake kwa lugha ya Kiswahili
hivyo huchangia sana katika kueneza Kiswahili.
Pia vyombo vya habari
vilijishughulisha sana katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili. Vyombo
hivyo ni kama magazeti na radio. Miongoni mwa magazeti yaliyojishughulisha sana
na uandikaji wa Makala mbali mbali yanayohusu lugha ya Kiswahili ni kama
Msimulizi (1888), Habari za mwezi (1894), Pwani na Bara (1910) Rafiki yangu
(1890), Habari leo (1954), Kiongozi (1950) Mwangaza ( 1923), Sauti ya pwani
(1940) na Mazungumzo ya Walimu wa Unguja (1954) n.k. Baadhi ya magazeti hayo
kulikuwa na ukurasa maalumu unaohusu taaluma ya lugha ya Kiswahili. Gazeti
Mambo leo liliandika mashairi na hadithi mbali mbali za fasihi simulizi. Kwa
upande wa redio Tanganyika ilianzisha matangazo yake kwa kutumia lugha ya
Kiswahili mnamo miaka ya 1950. Wakati wote redio iliendelea kutangaza matangazo
yake kwa Kiswahili. Hii kwa kiasi kikubwa ilichangia kukuza na kueneza
Kiswahili Tanzania.
Maendele ya lugha ya
Kiswahili yalichukuwa sura mpya mara tu baada ya uhuru. Harakati
zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania zilipelekea maenedeleo makubwa ya lugha
ya Kiswahili. Mnamo mwaka 1964 lugha ya Kiswahili iliteuliwa kuwa lugha ya
Taifa. Lugha hii ilitumika katika shughuli zote za kitaifa. Massamba na wenzake
(2004) “ mikutano yote iliyohusiana na wananchi mijini na vijijini iliendeshwa
kwa lugha hii ya taifa”. Hivyo Kiswahili kilihimizwa kutumika katika
mawasiliano yote hususani katika shughuli za umma na Wizara zote pamoja na
Bunge.
Jambo jengine
lililopelekea maendeleo ya lugha ya Kiswahili baada ya uhuru ni kuudwa kwa
vyombo mbali mbali vya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo
vilikuwa na majukumu makubwa kama vile kuendeleza usanifishaji lugha, kuunda
istilahi na kutaarisha viiarida na vitabu ambavyo viliweza kusaidia waswahili
na wale ambao wanifunza lugha ya Kiswahili. Mfano wa vyombo hivyo ni BAKITA, TAKILUKI,
BAKIZA, BAMITA, UWAKIVITA na kadhalika. Vyombo hivi vilisaidia sana maendeleo
ya Kiswahili kutokana na kazi zao kwa kila chombo (Massamba na wenzake 2010) Kuanzishwa
kwa vyombo mbali mbali vya habari viliendelea kutumia Kiswahili kwa kiasi
kikubwa vyombo hivyo ni magazeti, majarida, radio, na runinga. Ambavyo
vilitangaza kwa lugha ya Kiswahili. Mifano ya redio hizo ni kama radio Nuru,
Adhana, Radio one, Redio Free Afrika n.k. Mifano ya runinga ni ITV, Star TV.
ZBC, TBC na nyenginezo.
Pia Kiswahili kinaendele
kutumika katika shughuli za elimu katika shule za msingi kama ni lugha ya
kufundishia na sekondari na vyuo vikuu
ambavyo wanatoa shahada mbali mbali pamoja na uzamini na uzamivu wa
somola kiswahili. Kiswahili kiliendelea kutawanya mawanda yake barani Afrika na
duniani kwa ujumla.
Elimu ya watu wazima ambayo huwajumuisha watu wazima kusoma
na kuandika.Watu hawa hujifunza kiswahili nakupelekea kuweza kusoma nakuandika
na kuzungumza kwa lugha ya kiswahili fasaha. Masamba (2010) anasema “nchini
kote elimu ya watu wazima imefundishwa kwa kiswahili kupitia masomo tofauti
kama vile ufundi, siasa, kilimo, na afya. Hali hii ilisaidia maendeleo makubwa
ya Kiswahili hapa nchini. Licha ya hayo maendeleo ya Kiswahili yanakuwa na
kuenea sehemu mbali mbali kwa kupitia shughuli za biashara, shughuli za
kisiasa, uchapishaji wa vitabu vya sarufi na fasihi, shughuli za utamaduni
pamoja na harakati mbali mbali.
Ukuaji na ueneaji wa
Kiswahili duniani Msokile, M (1992) anadai kuwa lugha ya Kiswahili hivi sasa
imepenya sehemu nyingi duniani. Kiswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki nzima,
Somalia, Msumbiji, Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Angola, Zaire, Zambia, Ruwanda,
Burundi, Nigeria, Sudan na Misri. Nje ya Afrika kuna vyuo vikuu, vituo vya
redio na televisheni vinavyoshughulikia lugha ya Kiswahili. Mfano wa vituo vya
redio ni Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran katika nchi ya Iran, Redio ya China
Swahili, BBC Swahili London. Inasemekana hivi sasa kuwa kuna watu zaidi ya
milioni 1000 wanzungumza Kiswahili duniani. Ushahidi wa hayo tunaona kuwa Papa
John wa pili alitembelea Tanzania mnamo
tarehe 1/06/1990 alitumia lugha ya Kiswahili. Pia Kiswahili sasa kinaendelea
kutumika katika kutafsiri nyaraka mbali mbali, mitandao au tovuti, sharia,
biashara, na uhakiki wa maandishi kuanzia wakati huo hadi sasa.
Pamoja na umaarufu wa
lugha ya Kiswahili dunia, lakini bado lugha hii inaendelea kukukabiliana na
changamoto nyingi. Kwa mujibu wa Dafina ya Kiswahili (2014) wamebainisha
changamoto kama zifuatavyo;
Katika dhana ya Kiswahili
bado kuna baadhi ya watu wanaonasibisha kiswahili na dini ya kiislam hili
limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa watumiaji wa lugha hii.
Pia upinzani mkubwa
kutoka katika lugha ambazo zimekwisha jitanua katika dunia, mfano Kiingereza,
Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Watumiaji au watu wenye asili na lugha hizo
wanakipiga vita kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitazimeza lugha
zao.
Kudharauliwa kwa
lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha za kigeni kwamba ndio pekee
zinazofaa kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hivyo Kiswahili
kuonekana kuwa hakifai kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kasumba mbaya na mtazamo
hasi katika lugha ya Kiswahili ambao unawafanya watu kukitukuza zaidi Kiingereza
na kutojua kuwa kiingereza ni sawa na lugha nyingine tu.
Kucheleweshwa kwa
maamuzi ya sera ya kukipa hadhi kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika
nyanja zote za elimu, na kiingereza kuwa somo tu. Hivyo inarudisha nyuma
maendeleo ya Kiswahili.
Wasomi wengi kuwa
nyuma katika kufanya tafiti mbalimbali juu ya lugha ya Kiswahili ili kuona ni
jinsi gani tunaweza kufunguka kiakili na kufahamu umuhimu wa kuwa na lugha ya Kiswahili.
Uchumi mdogo nao
unakwamisha kwa sehemu kubwa maendeleo ya haraka ya lugha ya Kiswahili duniani.
Kwa kuwa nchi nyingi zinashindwa kuzalisha wataalamu wengi wa lugha hii, pia zinashindwa
kufasiri maandiko kutoka lugha nyingine kuwa katika lugha ya Kiswahili kwa
sababu ni ghari mno.
Wazawa wa lugha hii wanakosa
moyo wa kuthamini na kujali tamaduni zao ambapo Kiswahili ni lugha inayotangaza
utamaduni wao lakini wao wanathamini sana utamaduni wa kimagharibi. Kwa hakika
hii ni changamoto kubwa ambayo inakikumba Kiswahili katika harakati zake za
kujitanua duniani kote.
Pia kuna dhana kuwa
Kiswahili ni lugha ya watu duni kitaaluma mathalani watu walioishia darasa la
saba. Hivyo hufanya watu kutaka kujifunza Kiingereza. Hii ni dhana ya watu
potofu kabisa ambayo inajitokeza kwa watu ambao ni wasomi kabisa.
Kwa upande wa
matumizi ya lugha ya Kiswahili, kumekuwa na matatizo makubwa ya kutumiwa
isivyosahihi na matumizi yasiyofasaha katika nyanja zake za kimatamshi,
kimaandishi na kimaana. Matatizo hayo ndiyo yanayopelekea kutokuwa na Kiswahili
sahihi na fasaha. Jambo la kusikitisha na kushtua zaidi ni kuwa kwa muda mrefu,
kumebaini na kuwa na Kiswahili sanifu lakini Kiswahili hiki kinazungumzwa na
kuandikwa kimakosa mno. Makosa haya hutendwa na taasisi mbalimbali zikiongozwa
na vyombo vya mawasiliano. Mfano katika magazeti waandishi wanatumia lugha inayokiuka
misingi na kanuni za Kiswahili sanifu tunachokielewa au wanachofundishwa
wanafunzi.
James, J. na
Faustino, M. (2011). Wameelezea changamoto zinazoikabili lugha ya
Kiswahili ni kama; ukosefu wa utashi wa
kisiasa, uhaba wa wataalamu, kuwepo kwa Viswahili vingi, kasumba za kikoloni,
kupenda lugha za asili, uhaba wa fedha.
Kwa ujumla, historia
ya lugha ya Kiswahili ni dhana tete ambayo kila mtaalam huwa na mtazamo wake.
Ni vyema kwa wasomi na wadau wa Kiswahili kufanya utafiti wa kina juu ya
historia ya lugha ya Kiswahili ili kuondosha utata huo na kubaini ukweli wa
historia yake. Pamoja na maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani bado Kiswahili
kinakabiliwa na changamoto mbali mbali. Ni jukumu la wapenzi wa lugha hii
kuziangalia kwa kina changamoto hizo ili kuimarisha maendeleo yake.
MAREJEO
Maganga, C (1997) Historia ya Kiswahili. Dar-es-salaam.
Chuo kikuu huria.
Massamba na wenzake
(1999) Sarufi Miundo Kiswahili Sanifu
Sekondari na Vyuo: Dar-es-salaam
TUKI.
Massamba, D. (2002). Historia ya Kiswahili. Nairobi: The Jomo
Kenyata Foundation.
Masebo, J. A (2002) Kiswahili Kidato cha 3 na 4. Dar-es
–salaam Nyambari Nyangwine Publisher.
Msokile, M (1992) Historian a Matumizi ya Kiswahili.
Dar-es-salaam: Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.
but I put things off too much and never seem to get started. Thanks though.
ReplyDeletedWebsite directory