Kwa
mujibu wa Eagleton (1983: 1 – 8) Fasihi ni tokeo la masimulizi ya lugha
kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta
athari maalum.
Fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu inayojaribu kusawiri vipengele
vya maisha, na mahusiano na hisia za watu katika muktadha fulani (Mulokozi,
1996).
kwa mujibu wa Mazingwe 1991:18 & Siyambo
na Mazrui (1992) wanasema kwamba fasihi ya Kiswahili ni fasihi yote inayoelezwa kwa lugha ya
Kiswahili hivyo, wataalamu mbali mbali wameonesha kuwa kuna aina mbili za
fasihi ya Kiswahili nazo ni : Fasihi simulizi na fasihi Andishi.
Vile vile lugha ya Kiswahili asili yake ni
upwa wa Afrika mashariki inayozungumzwa zaidi na waswahili, yenye utamaduni
wake wa Kiswahili na pia iliyosanifiwa kutokana na mchanganyiko na lahaja.
Baada ya kuangalia maana ya fasihi na lugha ya
Kiswahili tunaangalia mswahili ni nani? Hii ni kwa sababu ikiwa lugha ya Kiswahili ipo bila shaka
waswahili pia wapo, haiwezekani
kabisa kuwepo kwa lugha ya Kiswahili
bila ya kuwepo waswahili .
Mswahili ni mtu yeyote ambaye anaishi
mwambao wa Afrika mashariki na visiwa vyake, anayezungumza Kiswahili ikiwa ni
lugha yake ya kwanza, aidha mswahili ni mtu aliyetokana na jamii ya watu wa mwambao wa afrika
Mashariki na kuendeleza utamaduni wa mswahili, hii ikiwa ni pamoja na kucngumza
lugha fasaha.
Kutokana na maelezo hayo ni dhahiri kwamba, madai ya
baadhi ya watu kuwa hakuna waswahili hayakubaliki. Pia historia ya lugha ya
Kiswahili inaendelea kueleza kuwa waswahili wapo na walikuwepo tangu karne nyingi,
walijiita kwa majina mbali mbali mfano waamu, Wapate, Wamvita, Wapemba,
Waunguja n.k. Hata hivyo waliunganishwa kwa lguha moja na utamaduni mmoja. Wataalamu
wanaendeleza kueleza kuwa waswahili walikuwepo tangu karne nyingi na wapo hadi
sasa wana lugha yao ya Kiswahili na bila shaka wanayo fasihi yao ya Kiswahili.
Fasihi ya
Kiswahili ilikuwepo tangu kuwepo kwa mswahili. Aidha baadhi ya fasihi ya
mwanzo kabisa ni pamoja na utenzi wa Fumo Lyongo na nyimbo
mbali mbali za shughuli za kijamii ambazo ziliimbwa kwenye sherehe, harusi,
jando na unyago au katika shughuli za kiuchumi kama vile shughuli za kilimo na
uvuvi.
Wataalamu wanaendelea
kueleza kuwa waswahili ni wenyeji wa mwambao wa kaskazini kuanzia Barawa
(Somalia) hadi Tanga, wenyeji wa mwambao wa kusini na visiwa vyake.
Kuenea kwa lugha
ya Kiswahili katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki kumeifanya lugha hiyo iwe
chombo cha fasihi ya watu wote wanaoitumia, hivyo basi fasihi ya Kiswahili na
lugha ya Kiswahili vilikuwepo na
vilitumika kwa karne nyingi zilizopita hadi sasa. Fasihi hiyo ndio
tutakayoita Fasihi ya Kiswahili (Siyambo na Mazrui – 1992).
Kutokana na
maelezo hayo ni dhahiri kuwa fasihi ya Kiswahili ilikuwepo tangu kuwepo kwa
lugha ya Kiswahili na hii inaonesha kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya historia
ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ni kama ufuatao
Kwanza, historia ya fasihi ya
kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili chimbuko lake ni upwa wa Afrika Mashariki. Historia inaonesha
kuwa fasihi ya Kiswahili chimbuko lake ni upwa wa Afrika Mashairki hii ni
kutokana kuwa hapo awali jamii kama
Wangoni, Waamu, Wapate, jamii hizi zilipatikana katika Upwa wa Afrika mashariki
ambapo hawakufahamu jinsi ya kuandika fasihi katika maandishi, kwa sababu
zilikuwepo fasihi zao za jadi katika mapokezi (yaani fasihi simulizi), hivyo
walipowasili Waarabu ndipo walipoanza kuandika fasihi zao katika maandishi. Na
kutokana na ushahidi huo inaonesha kuwa fasihi ya Kiswahili ilikuwepo tangu
zamani kabla ya kuja kwa wageni mfano wa fasihi hizo ni utenzi wa FumoLyongo,
mashairi ya Inkishafi nakadhalika. mfano wa utenzi wa Fumolyongo ni:-
Liyongo kitamkali,
Akabalighi rijali,
Akawa mtu wa kweli,
Na haiba huongea.
Kwa upande wa
historia ya lugha ya Kiswahili tunaona
pia chimbuko lake ni Upwa wa Afrika Mashariki, na haikuletwa, na wageni
kama nadharia nyengine zinavyodai isipokuwa inasemekana waliunganisha
lugha ambazo zilikuwepo na kuziita jina moja tu nalo ni Kiswahili. Hii
ni kutokana na ushahidi mbali mbali
unaoonesha kuwa lugha ya Kiswahili ilikuwepo tangu zamani na ilikuwa
ikizungumzwa na jamii mbali mbali za
Afrika Mashariki mfano Wapate, Wangoni na Waamu, kama ni jamii za awali
zilizozungumza Kiswahili. Hivyo kutokana na jamii hizo ushahidi kama wa tenzi
mbali mbali zilizopatikana ambazo zinaonesha kuwa kweli Kiswahili kilikuwepo.
Hivyo kutokana na ushahidi huo ni kweli
kuwa upo uhusiano kati ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha
ya Kiswahili.Kwa hiyo tunaona kuwa historia ya fasihi ya Kiswahili ndio
iliotumika kama ushahidi wa kuthibitisha kuwa kweli lugha ya Kiswahili chimbuko
lake ni upwa wa Afrika mashariki, kama wataalamu mbali mbali walivyothibitisha
kutokana na ushahidi madhubuti kama wa fumoliyongo.
Vile vile uhusiano mwengine ni
kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na waarabu
pamoja na Uislamu. Hii ni kutokana na historia ya fasihi ya Kiswahili
katika sehemu ambazo zilichimbuka fasihi ya Kiswahili kama jamii za wapate,
wangoni, Waamu, hawa hawakuweza kuandika fasihi katika maandishi na hivyo katika mwaka 1670 waarabu walipofika katika
Upwa wa Afrika Mashariki walianza kuandika katika maandishi na inaaminika kuwa
miongoni mwa maandishi ya mwanzo ni utenzi wa Hamziyya ambao uliandikwa mwaka
1670, ambao ulikuwa ni wa kidini. Hamziyya unahusu maisha ya Mtume Muhammad
(S.A.W) mfano:-
“Akusudia, Mustwafa
kwenda Madina
Makka jina lake,
zikaleta kushukuru mema”
Pia utenzi wa
Tambuka ambao umezungumzia juu ya vita vikali vya Uislamu wa mwanzo wa mfalme
Herekali wa Dola ya Warumi (Mulokozi, 1996). Mfano wa beti ya utenzi wa
Tambuka.
“Bismilahi kutubu
Jina la Mola wahabbu
Arra Amani eribu
Na arraimu ukyowa”
Pamoja na utenzi wa al- Inkishafi na utenzi wa
Mwanakupona (Mulokozi 1999). Mfano wa beti ya utenzi wa Mwanakupona
unaozungumzia dini ya kiislamu.
“La kwanda kamata dini
Faradhi usiikhini
Na sunna ikimkini
Ni wajibu kuitia……(ubeti
12
Vile vile, tenzi
ambazo zinazungumzia uislamu ziliendelea hadi wakati wa Muyaka bin Haji (1770 –
1840) na pia yeye ndie aliyebadilisha mtindo
huu wa kidini na akaanzisha wake ulikuwa unazungumzia mambo mengine
tofauti (na kama inavyosemekana yeye ndiye alioutoa ushairi msikitini na
kuupeleka sokoni).
Katika historia ya lugha ya Kiswahili
pia imeathiriwa na waarabu na pamoja na uislamu. Kwani historia ya lugha
inaonesha kuwa waarabu ndio walioanzisha maandishi ya Kiswahili kwa hati za
kiarabu pamoja na utamaduni wa
mswahili na ustaarabu wao unaohusishwa
na uislamu. Kutokana na mchanganyiko mkubwa uliokuwepo baina ya waswahili na waarabu katika utamaduni wao ni
dhahiri kuwa fasihi zao zilikuwa zinazungumzia uisilamu kwa sababu hizo ni dhahiri kwamba historia ya fasihi ya
Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili
zina uhusiano mkubwa kutokana na utamaduni wa Kiswahili uliodhihirishwa
na waarabu na uislamu ndio uliopelekea fasihi hizo za awali kuzungumzia zaidi
mambo ya uislamu. Hivyo kutokana na
historia ya fasihi ya Kiswahili
kuathiriwa na uislamu, ndio iliyopelekea kuwa fasihi za awali za
Kiswahili kuzungumzia zaidi masuala ya dini ya kiislamu na kupelekea katika
utamaduni wa lugha ya Kiswahili na waswahili kuwa ni wa kiislamu.
Uhusiano mwengine kati ya historia
ya lugha ya Kiswahili na historia ya fasihi ya kiswahili ni kukua na kuimarika zaidi katika maeneo mengi ambayo
kihistoria yalikaliwa sana na wageni
ukilinganisha na maeneo ambayo hayakukaliwa sana na wageni. mfano wa
maeneo ambayo yalikaliwa sana na wageni
ni Pate, Lamu, Mombasa, Zanzibari na Tanga (Samuel na wenzake 2013) .Katika
maeneo hayo kulitokea watu mbali mbali wenye vipawa vikubwa katika kazi nyingi
za fasihi na kupata umaarufu mkubwa sana
kote Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, mfano:-
Pate, walitoka washairi maarufu kama
vile Sayyid Abdalla bin Nassir Mwanakupona binti Msham, Nabhani, Fumoliyongo,
Ali Athumani Koti, Mohammed bin Sheikh Malaka.
Mombasa – Ahmeid
Nassor bin Bhalo .
Lamu – Muhamed
Abubakar Kijumwa, Ahmeid Sheikh Nabhan, Zahid bin Mngumi, Tanga – Hemed bin
Abdalla Albuhri, Ghulam Mabondo bin Mwinyimatano, Swaleh Kibwana na Shaaban
Robert.
Zanzibar – Siti
binti Saadi, Yahya Burhan, Said A. Mohammed na Shafi Adam Safi. Historia hii na
mahala wanapotoka wanafasihi hawa imeelezwa na Mulokozi na Sengo 1995.
Pia, historia ya fasihi ya Kiswahili
na historia ya lugha ya Kiswahili zimeibuka kupitia masimulizi. Historia ya
fasihi ya Kiswahili ilizuka kwa masimulizi ambayo yalikuwa yakitumia lugha ya
mazungumzo ndipo zikaibuka hadithi fupi fupi.
Kwa mujibu wa Holman (1992) anasema kwamba
hadithi fupi ni masimulizi mafupi ya kubuni katika mtindo wa nathari. Baadhi ya
fani ambazo ziliathiri kuchipuka kwa hadithi fupi ni ngano, hekaya, rara,
utendi na riwaya chuku.
Katika historia
ya lugha ya Kiswahili kuna ithibati ya kutumika Kiswahili kabla ya kuja kwa
wageni, kuna ushahidi wa kimasimulizi ambapo wenyeji waliweza kusimulia. Mfano
wa masimulizi hayo ni kisa cha Anzaruni kilichoandikwa na binti Lemba (1663), siri al – as – rar iliyoandikwa na Kadhi
Kassim bin Jaffar, pia wakati wa ukoloni kulikuwa na hadithi za Wayunani(1889),
Mchawi(1900), H.R Haggad na safari za wasafiri (1925). iliyoandikwa Bunjan.
Hivyo basi uhusiano baina ya
historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ziliibuka
kupitia masimulizi. Mfano:- tendi, rara, hekaya riwaya chuku ambazo walikuwa
wakizisimulia,
Pia,
uhusiano mwengine uliojitokeza ni
kwa kukua kwa matumizi ya lugha. Lugha imeanza mara tu, mwanaadamu alipoanza kuyakabili
mazingira yake katika nyanja za kiuchumi na
kijamii. Hicyo watu walikuwa wakiitumia lugha katika shughuli mbali
mbali. Kwa minajili hiyo tunaweza kusema kwamba historia ya lugha ya Kiswahili
ndio iliyopelekea kuibuka kwa fasihi ya Kiswahili. Mfano kupitia katika jamii
walikuwa wakitumia nyimbo kama vile wimbo wa “Nabhan” mfano.
“Ndiwa wangu, Sindiwa wa mabaoni.
Ndiwa wangu, Ni mweupe wa Launi.
Ndiwa wangu Ushabihi wa peponi.”
Kwa upande wa
kiuchumi kulikuwa na wimbo wa “WAWE”
Wawe – Ni utungo
ambao huimbwa kwa kujitayarisha na shughuli za kilimo mfano wa beti wa ushairi
ni:-
“N’kasiye, N’kalima , N’kavuna.
Masika yenye makame, Chini yaliyojificha.
N’kafyeka, N’kachoma, moto ukajirimbika”.
Hivyo, tunaona wazi kwamba historia ya fasihi ya
Kiswahili inaonekena zilizuka kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii
ndipo tunapopata uhusiano mkubwa baina
ya historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili.
Hata hivyo, uhusiano uliopo baina ya
historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya lugha ya Kiswahili ni kwamba
zote ni fasihi ambazo huonesha sehemu ya utamaduni wa jamii kama vile
historia ya lugha ilivyo sehemu ya
utamaduni yenye kueleza au kuitazamia jamii kiutamaduni, kiuchumi, kiufundi na
kisiasa vile vile uhusiano huu huwa ni
darubini ya kuitazama mfumo wa maisha ya jamii yoyote ikiwa ni ya kikabila au
ya kibepari au ya kijamii.
Kwa kuhitimisha
suali letu, tunaweza kusema kuwa historia ya fasihi ya Kiswahili na historia ya
lugha ya kiswahili zina uhusiano mkubwa na kwamba dhana mbili hizi haziwezi
kutenganishwa kutokana na ukweli kwamba zinategemeana kwa kila hali,
zinajengana na kuathiriana sana . Kuwepo kwa
dhana moja kulipelekea kujitokeza kwa dhana nyengine. Hivyo ndio kusema
kwamba ,ni rahisi kuisoma na kuielewa historia ya fasihi ya Kiswahili iwapo
tutaisoma na kuielewa historia ya lugha ya Kiswahili kama vile ambavyo ni
rahisi kuisoma na kuielewa historia ya lugha ya Kiswahili iwapo tutaisoma na
kuielewa historia ya fasihi ya Kiswahili.
MAREJEO
Samwel ,M &
Seleman A,J &Kabiero A,J(2013) Ushairi
wa Kiswahili :Nadharia ,mwongozo kwa
walimu wa Kiswahili na diwani MEA, DSM .MVP
TUKI(1983) Makala za seminar za kimataifa ya waandishi
wa Kiswahili 111-Fasihi, DSM:DUP
Mulokozi,M,M(1999)
Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili
Dar-es-Salaam :chuo kikuu cha Dar-es- Salaam
Mulokozi ,M,M
(19 96)utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili
Dar-es-Salaam:Tuki
Maganga,C(1997) Historia ya Kiswahili
,Dar-es-Salaam:Chuo kikuu huria cha Tanzania
Mmefanya kazi nzuri ambazo zinatuelekeza kujua Kiswahili nchini Rwanda
ReplyDelete